Afya ya uzazi, stadi za maisha na michezo

Kitabu hiki kimeandikwa kwa makusudi ya kuwasaidia vijana wa kiume na wa kike kuchukua mwelekeo unaofaa ili waweze kufanikiwa katika maisha yao. Maisha ya zama hizi yanatofautiana sana na maisha ya zama zilizopita kulipokuwa na vyanzo vichache vya taarifa, mawasiliano na mwingiliano mdogo wa watu wenye asili ya jamii tofauti. Kutokana na kukua kwa sayansi na teknologia mwingiliano wa watu wa jamii tofauti umeongezeka sana. Aidha vyanzo vya habari na mawasiliano vimekuwa vingi na habari husambaa kwa haraka sana kutoka sehemu moja hadi sehemu nyingine. Vyanzo hivi vya taarifa hutoa fursa kwa vijana wengi kuweza kunufaika. Kwa upande mwingine hupata changamoto nyingi katika maisha yao. Mwingiliano wa watu na upatikanaji wa habari nyingi tofauti na jamii yaohuapatia chanagamoto vijana wengi yakutojua waishi kwa kufuata kanuni na misingi ipi ya maisha. Hii ni kwasababu wale wanaotamani kuishi kisasa kwa misingi ya utandawazi wanajikuta hawana taarifa na raslimali za kutosha kuwawezesha kuishi hivyo. Pia wale wanaotamani kuendeleza mila na desturi za zamani wanajikuta hawana misingi yote ya kuwawezesha kuishi hivyo kwani muktadha uliowawezesha mababu kuendesha maisha kwa misingi ya mila na desturi hizo imebadilika sana.

Kitabu hiki kimeandikwa ili kuwasaidia vijana kukabiliana na aina hii ya mkanganyiko ambao unawafanya kuonekena kutokuwa na muelekeo thabiti katika maisha. Athari zinadhihirika kwa hali mbalimbali mfano mimba za utotoni, ndoa zinazovunjika baada ya kudumu kwa muda mfupi sana, kuvaa mavazi yasiyoweza kusitiri maumbo ya miili yao, uzururaji ovyo, kutokupenda kazi na utumiaji vileo vikali na madawa ya kulevya.Yote hayo hupelekea utoro na kutofanya vizuri shuleni, na mambo mengine mengi yasiyofaa ambayo mengine hayastahili kuandikwa katika kitabu hiki azizi. Athari zinadhihirika kwa hali mbalimbali mfano mimba za utotoni, ndoa zinazovunjika baada ya kudumu kwa muda mfupi sana, kuvaa mavazi yasiyoweza kusitiri maumbo ya miili yao, uzururaji ovyo, kutokupenda kazi na utumiaji vileo vikali na madawa ya kulevya.

Kitabu hiki kinalenga kuwaelimisha vijana waweze kujitambua na kutambua mazingira yanayowazunguka ili waweze kuchukua hatua sahihi kwa wakati sahihi kabla hawajachelewa na kujikuta wameingia kwenye matendo au tabia zisizofaa.

Kitabu hiki kina jumla ya mada kumi na tano (15). Kila mada imegawanyika katika mada ndogo kadhaa kutegemeana na wingi wa maudhui katika mada husika. Kwahiyo kitabu kizima kina jumla ya mada ndogo thelathini na nne (34). Aidha kila mada ndogo imetengewa muda unaotarajiwa kutumika kuifundisha. Muda uliowekwa ni makadirio tu. Mwezeshaji anaweza kuongeza au kupunguza kwa kadiri ya muktadha ambapo mada ndogo itatolewa. Zingatia kwamba msingi wa uwezeshaji wa mada zote utakuwa kwa vitendo hivyo muda usipunguzwe kiasi cha kuwapunguzia walengwa muda wa kujifunza kwa vitendo na wala usiongezwe muda mwingi kiasi cha kuwafanya walengwa kuchoka na kupoteza hamu ya kujifunza. Kutegemeana na muktadha wa kutolea elimu hii mwezeshaji anao uhuru wa kuanza kuwezesha mada yoyote anayoona ina umuhimu wa pekee au ndio inayopasa kuanza ili washiriki wa muktadha huo waweze kumudu mada hiyo vizuri.

Kwa mtiriko wa mada ndogo katika kila mada kuu ni lazima ufuatwe kama ulivyo katika kitabu kwa kuwa mada ndogo linayotangulia katika kila mada kuu linajenga msingi wa kuelewa mada nyingine inayofuata.

Kwa upande wa walengwa wana uhuru wa kushiriki katika kujifunza mada ambayo yeye anaiona itamsaidia katka maisha yake. Mshiriki halazimiki kushiriki mada zote lakini mwezeshaji akiweza kuwashawishi walengwa kushiriki katika mada zote itakuwa vizuri sana, na kwa hakika haya ndio makusudi ya kitabu hiki.

Aidha, mwishoni mwa kila mada ndogo kuna sehemu ya muongozo kwa mwezeshaji. Madhumuni ya sehemu hizi ni kumdokeza mwezeshaji mwelekeo wa maarifa yanayopaswa kutolewa katika mada ndogo husika. Maelezo haya yapo mwishoni mwa kila mada, hivyo inashauriwa ni lazima mwezeshaji asome mapema kabla ya kuanza kufundisha ili pale inapobidi aweze kutafuta maelezo ya ziada yatakayomwezesha kuendesha somo kwa umahiri unaomstahiki mwezeshaji.

Kitabu hakitoi jawabu la moja kwa moja kwa maswali mbalimbali wala hakijaweka kanuni zisizopaswa kuvunjwa, kuongezwa, wala kupunguzwa kwa namna yoyote ile juu ya nini vijana wanapaswa kufanya ili kuendesha maisha yanayotia tumaini la mafanikio. Kitabu hiki kitawasidia sana vijana kutambua mengi mema na bora kuhusu maisha yao kwa kupata fursa ya kujifunza yaliyomo katika kitabu hiki.

Asante

Dr. A. Ngalawa